Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imetoa mafunzo maalum ya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini kwa wawezeshaji ngazi ya halmashauri, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia TASAF.
Mafunzo hayo yametolewa na wawezeshaji kutoka TASAF Makao Makuu kwa lengo la kuwajengea uwezo wawezeshaji wa halmashauri katika kusimamia kikamilifu zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini chini ya Reforms Measure Namba 4 inayotekelezwa na Serikali kupitia TASAF.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Dkt. Christopher Semanyanza alisisitiza umuhimu wa uwazi, uadilifu na uzingatiaji wa miongozo wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo ili kuhakikisha linafanyika kwa haki na bila ubaguzi wa aina yoyote.
Katika kuimarisha maadili ya utumishi wa umma, washiriki wa mafunzo hayo waliapa kiapo cha maadili kilichoongozwa na Mwanasheria wa Serikali Wilaya ya Nzega, Bw. Patrick Muhere, wakiahidi kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Nzega, Bi. Jovita Patrick amesema lengo la maboresho hayo ni kupanua masijala ya walengwa ili kuhakikisha kaya maskini pamoja na kaya zilizo katika hatari ya kuingia kwenye umasikini zinatambuliwa mapema na kujumuishwa kwenye mpango madhubuti wa msaada.
Amesema kanzidata hiyo itaiwezesha Serikali kuwafikia walengwa kwa haraka na kwa ufanisi pindi majanga au changamoto zitakapojitokeza.














Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa