MAZINGIRA MAZURI NDIYO YATAKAYOPELEKEA WATUMISHI KUBAKI
Posted on: October 18th, 2018
Uwekaji wa mipango mizuri na inayotekelezeka ndiyo itakayopelekea kuinua kiwango cha elimu katika mkoa wa Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe.Agrey Mwanri aliwasisitiza viongozi wote katika Mkoa wake kuwa mazingira mazuri ya kufanyia kazi hasa kwa watumishi yatasaidia na kupelekea kuinua kiwango cha Elimu katika mkoa wa Tabora. Aliyasema hayo mara alipokuwa akifungua kikao kazi kwa walimu wakuu,wakuu wa shule na maafisa elimu kata wa halmashauri ya wilaya na Mji jana katika ukumbi wa chuo cha maendeleo Uchama.
Wakati mwingine walimu wamehamishwa kutoka eneo A kwenda eneo B lakini wasilipwe eti kwa sababu maeneo hayo hayana umbali wowote. Inakuhusu nini kama ni haki yake mtumishi huyo? Alisema mkuu wa Mkoa. Na kama hakuna fedha taarifa ama elimu itolewe kwa watumishi kuwa uhamisho utafanyika na namna ya malipo itakavyolipwa. Hizo ndizo motisha kwa walimu kwani Serikali haiwezi kugawa fedha kwa kila mtumishi anayefanya kazi vema.
Akiongea katika kikao hicho mkuu wa mkoa alisisitiza kuwa haiwezekani yeye kuongoza mkoa mkubwa lakini wenye mambo ya ovyo, kama mkoa kuwa na watoto wasiohudhuria shule (utoro), mimba za utotoni na kuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa upande wa elimu.
Alisema ‘’Watu wanapenda ujisikie kuwa huna akili ili wakutawale sawa na watu wenye fedha na matajiri wanaweza kusema maneno ya hovyo pasipo kujali kama duniani kuna binadamu. Watu wote duniani wana akili’’ akiendelea kusema mkuu wa mkoa alitoa mfano kuwa bibi kizee anaweza kupata shahada lakini baada ya miaka thelathini. Alisisitiza kuwa ili tuweze kuwa na mafanikio lazima tufanye kazi kwa muda wa ziada, ‘’ndiyo tunaweza” kwa mwanzo huu na ufaulu uliooneshwa kwa miaka hii ya karibuni kutoka mkoa wa mwisho na kufikia kuwa wa tatu kitaifa kwa matokeo ya kidato cha nne na matokeo ya darasa la nne tukaongoza.
Uanzishwaji wa shule katika maeneo ya hifadhi na yasiyo stahili na pasipokupata kibali toka kwa mkurugenzi, shule ‘’kanjanja’’zimeanzishwa kwa wingi na kupelekea wanafunzi wengi kumaliza darasa la saba pasipo kujua kusoma na kuandika. Shule hizo huanzishwa na wazazi na walimu wake hutoka miongoni mwa jamii husika na pasipo kupata mafunzo yoyote hivyo basi mkuu wa mkoa alimwagiza katibu tawala wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Nzega kuwa ikiwa shule iliyojengwa katika maeneo yasiyo na sifa basi na ifutiliwe mbali.
Akizungumza juu ya motisha kwa watumishi Mhe. Agrey Mwanri alisema kuwa wapo walimu wanatumia muda wa ziada kuwaandaa watoto mpaka saa nne za usiku na wanafahamika hao ndiyo wa kuwapa vyeo.