Mafunzo ya kuwajengea uwezo Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Nzega na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega yamehitimishwa leo kwa msisitizo mkubwa juu ya matumizi sahihi ya Teknolojia (TEHAMA) pamoja na kuzingatia maadili katika uongozi na utumishi wa umma.
Katika siku ya tatu na ya mwisho ya mafunzo hayo, Madiwani wameelekezwa kutumia TEHAMA kama nyenzo ya kuongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, huku wakikumbushwa kuwa matumizi ya teknolojia bila kuzingatia maadili yanaweza kuathiri maendeleo yanayokusudiwa.
Mafunzo hayo pia yameweka msisitizo kwa Madiwani kutambua mipaka ya majukumu yao, kwa kuelekezwa kutokuingilia kazi za kitaalamu zinazotekelezwa na wataalamu wa Halmashauri, ili kulinda weledi, uwajibikaji na ubora wa maamuzi katika utekelezaji wa majukumu ya umma.
Akiwasilisha mada ya maadili, mkufunzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ameeleza umuhimu wa viongozi wa umma kujiepusha na migongano ya maslahi, akifafanua kuwa kiongozi hapaswi kushiriki katika maamuzi au michakato inayohusisha maslahi yake binafsi au ya watu wa karibu, kwani hali hiyo huathiri utekelezaji wa wajibu wake kwa manufaa ya umma.
Aidha, ilielezwa kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inawataka viongozi kuzingatia uadilifu na kujiepusha na mahusiano ya kibiashara yanayoweza kuathiri uwajibikaji wao. Kwa mujibu wa sheria hiyo, kiongozi wa umma hapaswi kuingia au kushiriki katika biashara au mikataba na Halmashauri anayoihudumia au yenye mamlaka juu yake, ili kuepuka mgongano wa maslahi na kulinda maslahi ya umma.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamehitimishwa kwa wito kwa Madiwani kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuimarisha uongozi, kuzingatia maadili, na kutumia TEHAMA kwa njia itakayochochea maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wa Nzega.










Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa