Timu ya wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, kwa kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, leo imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya elimu inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega.
Ukaguzi huo umefanyika katika Kata ya Nata pamoja na Shule ya Msingi Katangwa iliyopo Kata ya Mambali, ambapo timu ilikagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, ofisi za walimu, vyoo, pamoja na majengo ya shule za awali za mfano yanayolenga kuboresha mazingira ya malezi, ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto wa awali.
Ziara hiyo imelenga kujiridhisha na ubora wa utekelezaji wa miradi ya elimu, matumizi sahihi ya fedha za Serikali, pamoja na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha (value for money) na kukamilika kwa wakati uliopangwa ili kuboresha sekta ya elimu ndani ya halmashauri.
Timu ya ukaguzi imejumuisha wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora wakiwemo Ramadhan Mpolanje (Mchumi), Pelagia Tiliya (Muhasibu), Alex Mhanga (Afisa Biashara) pamoja na Magesa Amos (Wakili wa Serikali), wakishirikiana kwa karibu na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega.
Halmashauri ya Wilaya ya Nzega inaendelea kutekeleza kikamilifu sera, mipango na miongozo ya Serikali katika kuboresha sekta ya elimu, huku ikitambua na kuthamini mchango wa ufuatiliaji na tathmini unaofanywa na mamlaka za juu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyokusudiwa na kuleta manufaa kwa wananchi.








Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa