Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Akabidhi Mikopo yenye Thamani ya Shilingi 84,000,000
Posted on: February 18th, 2019
Mwenyekikiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Mhe. Kiwele Michael Bundala amekabidhi mikopo kwa vikundi 52 ikiwa wanawake vikundi 32 na vijana vikundi 20. Zoezi hilo limefanyika leo katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kwa Kukabidhi Shilingi Milioni themanini nan ne.
Akisoma risala kwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya Ndugu Robert Mwanga alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19 Halmashauri ina mpango wa kutoa mikopo kufikia kiasi cha shilingi 225,140,000/= ikiwa vijana ni Shilingi 88,040,000/=, wanawake 88,040,000/= na walemavu ni shilingi 49,000,000/=. Alisema kuwa fedha hii inatoka katika mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha sawa na asilimia 10 ya mapato yote.
Aidha afisa huyo alionesha mafanikio kuwa ni pamoja na kutoa kiasi cha shilingi milioni 132,500,000/= mpaka kufikia robo hii ya tatu ambayo ni sawa na asilimia 59% ya lengo la mwaka huu wa fedha. Leo hii vikundi vikundi 20 vya vijana vimepata kiasi cha shilingi 42,000,000/= na vikundi vya kinamama kiasi cha shilingi 42,000,000/= kufanya jumla ya shilingi 84,000,000/=.
Halmashauri imefanikiwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya elimu ya ujasilamali,uibuaji miradi pamoja na uendelezaji wake. Mpaka kufikia robo ya tatu vikundi 89 vimenufaika na mikopo hiyo sawa na ongezeko la asilimia 83% ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita.
Akielezea matatizo yanayojitokeza katika zoezi hilo ni pamoja na vikundi vya walemavu kutojitokeza kuomba mikopo,ucheleweshaji wa marejesho kwa baadhi ya vikundi,uhaba wa rasilimali fedha na maombi ya mikopo kuwa makubwa kuliko fedha iliyopo. Mahitaji ya vikundi ni kiasi cha shilingi = 206,000,000/= uwezo wa halmashauri ni kiasi cha shilingi 184,000,000/- sawa na silimia 41% ya maombi yote.
Akihitimisha risala hiyo Kaimu Maendeleo ya jamii Wilaya ndugu Robert Mwanga alimuomba mwenyekiti kutumia nafasi yake kuwashawishi waheshimiwa madiwani kuwahamasisha wananchi kuwa na moyo wa kurejesha kwa wakati ili kutoa nafasi kwa wananchi wengine kuweza kukopa.
Aidha Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Mhe. Kiwele Michael Bundala aliwasisitiza wanavikundi kuwa na matumizi mazuri ya fedha, “serikali imetoa fedha hii ili kuwafanya wananchi wake kuufikia uchumi wa kati’’ hivyo aliwataka waitumie fedha hiyo kwa faida kubwa, wala hawakupewa fedha hiyo kwa maana ya kununua chakula nyumbani,kwenda baa, kusuka nywele na kununua vitenge. Aliwaomba wasimamie malengo yote waliyojiwekea ili kuleta tija.
Akiendelea kuongea Mheshimiwa Kiwele alisema kuwa walemavu si wengi kutoka maeneo ya kata moja hivyo tutaandaa utaratibu wa kuwapata ili watumie fursa hii katika kuzalisha kuliko kukaa bure. Pamoja na hayo Mhe. Alisisitiza kuwa vikundi vingi vimekuwa na maandiko yanayofanana hivyo aliwaomba wawe na ubunifu katika kuandaa maandiko.
Akisema na wananchi hao aliwataka wanavikundi wote watakaofanya marejesho vizuri ndani ya miezi 6 watapewa kipaumbele katika kupewa mikopo mingine.
Kwa upande wa wanavikundi wao waliishukuru serikali kwa namna inavyowajali wananchi wanyonge.
Mkurugenzi mtendaji(W) ndugu Sekiete S Yahaya aliwaasa wanavikundi kutotumia vibaya fedha hizo, tumieni taratibu mlizojiweka katika kutumia fedha hizo,’ alisema mkurugenzi. Katika kuhitimisha kikao hicho Mkurugenzi alisema kuwa katika kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi mikopo hii si kama sadaka msikitini ama kanisani hii ni fedha unayopewa ili uirejeshe na ndiyo maana fedha hii haina riba kwa asilimia miamoja.aliwataka wananchi kutumia vizuri mikopo hii ili kuondoa umasikini na kuwa na uwezo wa kujitegemea. Aliahidi kuwa pamoja na kupewa mikopo hii kama taasisi haitaishia hapo bali ni pamoja na kuwatembelea huko walipo. Aliwatakia utendaji mwema katika shughuli zao.