Leo tarehe 27 Januari, ikiwa ni siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mheshimiwa Naitapwaki L. Tukai, ameazimisha siku hii muhimu kwa vitendo vya kijamii vinavyoakisi utu, uzalendo wa kweli na uongozi wa mfano.
Katika kuenzi maono na mchango mkubwa wa Rais Samia katika kuimarisha sekta ya elimu na utunzaji wa mazingira, Mheshimiwa Tukai alitembelea Shule ya Sekondari Ikindwa, iliyopo Kata ya Ikindwa, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Ziara hiyo ililenga kuhamasisha wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa elimu, malezi bora na kulinda mazingira.
Katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya alishirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Bukene, ambapo Mheshimiwa Mbunge John Luhende aliwakilishwa na Katibu wake, Bw. Abubakary Bukuku. Kupitia ushirikiano huo, waliweza kukabidhi zawadi mbalimbali za kielimu kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, zikiwemo madaftari, kalamu, mpira kwaajili ya wavulana na wasichana,mabegi ya shule, rula pamoja na sare za shule. Zawadi hizo zilitolewa kama sehemu ya kuwahamasisha wanafunzi kuendelea na masomo pamoja na kupunguza mzigo kwa wazazi na walezi.
Mheshimiwa Tukai alitumia fursa hiyo kutoa onyo kali kwa wazazi na walezi wanaowazuia watoto kwenda shule, akisisitiza kuwa kitendo cha kuwanyima watoto haki ya elimu ni kosa la kisheria. Alieleza wazi kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa mara moja dhidi ya yeyote atakayebainika kuwakatisha watoto masomo, kuwaozesha mapema, kuwapeleka kufanya kazi za mashambani, kuchunga mifugo au kuwatumikisha katika kazi za ndani.
Aidha, aliwahimiza wanafunzi kutoa taarifa pindi wanapobaini kuwepo kwa mwanafunzi aliyepaswa kujiunga na Kidato cha Kwanza lakini amezuiwa na mzazi au mlezi wake. Alisisitiza kuwa Serikali ya Wilaya haitasita kuchukua hatua kali kwa mzazi au mlezi yeyote atakayekiuka haki za mtoto.
Katika kuendeleza ajenda ya taifa ya utunzaji wa mazingira, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya pamoja na maafisa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, walishiriki zoezi la upandaji wa miti ya kivuli na matunda katika eneo la shule hiyo. Alitoa wito kwa walimu na wanafunzi kuitunza miti hiyo kama sehemu ya kulinda mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Baada ya kukamilisha shughuli za kijamii shuleni, Mheshimiwa Tukai alirejea ofisini ambako alikata keki maalum kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Keki hiyo ilitolewa na wafanyabiashara wa Wilaya ya Nzega kama ishara ya kutambua mchango mkubwa wa Rais Samia katika kuwawezesha wafanyabiashara na kuimarisha mazingira bora ya biashara nchini, sambamba na kumtakia maisha marefu, afya njema na mafanikio endelevu katika kulitumikia Taifa.
Maadhimisho haya yamebeba ujumbe mzito unaoonesha kuwa uzalendo wa kweli unaanza kwa vitendo, kwa kulinda haki za watoto, kuwekeza katika elimu na kutunza mazingira yetu.
Mti wa leo ni maisha ya kesho, ni mvua ya kesho, ni maji ya kesho, na ni ardhi salama ya kesho. Anza sasa, mhimize na mwingine.
“Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti”
#MazingiraNiUtu
MATUKIO KATIKA PICHA






















Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa