"Piga ua garagaza lazima kazi iendelee na hakuna kusimama" ameyasema hayo mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Nzega Wakili Kiomoni Kiburwa Kibamba alipokuwa kwenye ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa shule za Sekondari leo.
Mpaka kufikia saa moja jioni msafara wa wataalau wa halmashauri ukijumuisha wakuu wa Idara ulikuwa unaendelea kufanya ukaguzi huo kwa maeneo yote ya shule za sekondari.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji, Kiomoni K Kibamba amewataka wakuu wa shule zote kuhakikisha wanaweka taa usiku ili kazi iendelee usiku kucha hii yote imesababishwa na tabia ya wazabuni kuchukua tenda na kutoifanya kwa wakati,hivyo kumlazimu Mkurugenzi Mtendaji kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule,watendaji na viongozi wa kijiji kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha vyovyote iwayo ili kuhakikisha siku ya leo majengo yote ambayo hayakuwa yametandika jamvi kama,Mizibaziba,Nkiniziwa,Tongi,Budushi na Magengati yanafanya hivo.
Isitoshe watendaji wakishirikiana na jeshi la jadi la sungusungu wahakikishe wanatumika kubeba tofali na kuleta kokoto katika eneo la ujenzi ili kuepuka ulaghai wa wazabuni wanaoufanya kwa kuchelewesha kazi.
"Hakuna siku iitwayo kesho, kama kuna yeyote aliyewahi kukutana nayo aseme" aliyasema hayo alipokuwa shule ya sekondari Budushi baada ya kuonekana zoezi la ujenzi linasuasua, hiyo ikisababishwa na mzabuni aliyekuwa amechukua tenda kutoleta kokoto na mawe kwa wakati, hivyo kulazimika kuchukua hatua za kutafuta mzabuni mwingine ili kazi iendelee.
Katika ukaguzi huoMkurugenzi mtendaji alimtaka mkuu wa shule ya Magengati na mtendaji wa kijiji kuhakikisha wanaondoa tofauti zao na kujenga umoja ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati. Aidha Mwenyekiti wa kijiji hicho Bi.Halima Salumu Mseluka aliomba msamaha kwa ajili ya viongozi hao walioonekana kutofautiana na kurushiana mpira, baada ya kuonekana kuwa hapakuwa na uwazi juu ya taarifa za ujenzi tofauti na Mwalimu mkuu shule ya sekondari Milamboitobo ambaye alibandika taarifa za matumizi ya fedha ubaoni kwamba kila mmoja anaweza kuona na kusoma.
Shule za Kampala madarasa 3, iPuge madarasa3 na Mwanhala madarasa 3 yalikuwa yamefikia hatua ya kuweka lenta.
Timu ya wakuu wa idara(CMT) imeendelea na zoezi la ukaguzi wa miradi usiku huu katika maeneo ya Karitu,Nata na Sigili.
Imeandaliwa na Isidori Mayagilo
ICTO
Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa