Kijiji cha Mwamalulu, Kata ya Nata, kimefanyika mdahalo wa vijana uliofanyika katika Shule ya Sekondari Nata, ukihusisha vijana zaidi ya 64 kutoka vijiji sita vya Kata ya Nata.
Mdahalo huo ulilenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu nafasi na fursa mbalimbali zinazowazunguka, umuhimu wa uzalendo, umoja na amani, pamoja na kuwahamasisha kutumia fursa hizo kwa maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla.
Akitoa mada katika mdahalo huo, Mtendaji wa Kata ya Nata, Fundi Kasim, alisisitiza umuhimu wa uzalendo, vijana kujitambua na kuzitambua fursa zinazowazunguka, pamoja na kuthamini na kulinda amani ya taifa letu. Alieleza kuwa endapo kijana atakutana na changamoto au mkwamo wowote, anapaswa kufuata njia sahihi ili changamoto hizo ziweze kutatuliwa badala ya kukata tamaa.
Kwa upande wake, Afisa wa Benki ya CRDB, Gloria Makweta, alielezea namna vijana wanavyoweza kujenga mahusiano na benki hiyo ili kufikia fursa mbalimbali za kifedha. Alibainisha fursa za mikopo ya pikipiki kwa vijana pamoja na mikopo ya vikundi kama njia ya kuwawezesha vijana kiuchumi.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Margwe Tsere, alisisitiza umuhimu wa vijana kuungana, kuunda na kusajili vikundi, akibainisha kuwa umoja una faida kubwa sana. Aliwahamasisha vijana kuchangamkia mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri, ambayo ni nafuu na haina riba, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Peter Mashimba, aliwataka vijana kuwa waaminifu, kufanya kazi kwa moyo na kwa weledi. Alisisitiza kuwa kijana asiye mwaminifu hujiweka mbali na fursa nyingi zilizopo. Aliongeza kuwa badala ya vijana kuelekeza lawama kwa serikali kwa madai ya kutowajali au kutowasikiliza, wanapaswa kutambua kuwa fursa zipo nyingi na zinahitaji juhudi, nidhamu na uadilifu kuzifikia.
Zaidi ya vijana 64 kutoka vijiji vya Kabale, Kanolo, Nata, Mwamalulu, Mwabangu na Kilabili, walipata nafasi ya kueleza changamoto zao, kutoa maoni pamoja na kuomba serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana kuendelea kuwapatia msaada na kuwaangalia vijana wa maeneo ya vijijini.
Mdahalo huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Emmy Ndolingo, Afisa Maendeleo wa Kata ya Nata; Shukuru Mbula, Mtendaji wa Kijiji cha Mwabangu; Mariam Zahoro, Afisa Afya wa Kata ya Nata; Gaudensia J. Tawa, Afisa Mtendaji wa Kata ya Nata; Witness D. Lembalai, Afisa Misitu wa Kata ya Kilabili; Maryciana D. Antony, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kabale pamoja na Kashindye Kamil, Afisa wa Benki ya CRDB.
Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa