Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Nzega na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega wameendelea na siku ya pili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo, wakipata elimu kuhusu dhana ya miradi shirikishi pamoja na mchakato wa mipango na bajeti, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega uliopo eneo la Ipazi na yamelenga kuwawezesha Madiwani kuelewa umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo, jambo linalosaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi na kuongeza uwajibikaji.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mwezeshaji wa mada alieleza kuwa faida za ushirikishwaji katika miradi ya maendeleo ni pamoja na kuongeza umiliki wa miradi kwa wananchi, kupunguza changamoto wakati wa utekelezaji na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
Katika mada ya mipango na bajeti, Madiwani walielezwa kuwa dhana hiyo inaeleza mchakato wa kutambua malengo ya maendeleo, kubainisha miradi ya maendeleo na kuweka vipaumbele kulingana na mahitaji halisi ya jamii, ili rasilimali zilizopo zitumike kwa tija na kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Aidha, Madiwani walihamasishwa kutumia maarifa waliyojifunza kuimarisha usimamizi wa miradi katika maeneo yao, kushirikiana na wananchi katika hatua zote za utekelezaji na kuhakikisha miradi inaendana na mipango ya maendeleo ya Halmashauri.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi tarehe 21 Januari, 2026, huku yakilenga kuongeza ufanisi wa Madiwani katika kusimamia maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Nzega.






Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa