Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora imefanya kikao maalumu kilicholenga kujadili na kupanga mikakati ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiutendaji na maendeleo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kikao hicho kimeongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Bw. Mwarami Seif, na kuhudhuriwa na wakuu wa divisheni na idara mbalimbali za halmashauri, pamoja na Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji kutoka maeneo yote ya wilaya.
Katika kikao hicho, wajumbe walijadili ajenda kuu mbalimbali ikiwemo kujifunza na kujisajili katika mfumo wa TAUSI unaotumika katika ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa mamlaka za wilaya, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Aidha, kikao kilijadili suala la uhuishaji wa rejesta za wakazi ili kupata takwimu sahihi zitakazosaidia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
Masuala mengine muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora za afya, pamoja na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama sehemu ya kuwawezesha kiuchumi.
Vilevile, kikao hicho kiligusia masuala ya kiutumishi yakiwemo nidhamu kazini, uwajibikaji wa watendaji katika ngazi zote, pamoja na mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Halmashauri ya Wilaya ya Nzega inaendelea kudumisha ushirikiano mzuri kati ya viongozi na watumishi wake kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi na kuhakikisha sera, mipango na miongozo ya Serikali inatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Nzega.
MATUKIO KATIKA PICHA















Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Kata ya Utwigu kijiji cha Mwambaha Lubisu )
Anuani ya Posta: S.L.P 4
Telephone: 026 2692349
Simu ya Kiganjani: 0765600994
Barua pepe: md@nzegadc.go.tz
Hati miliki Halmashauri ya Wilaya ya Nzega @ 2017. Haki zote zimehifadhiwa